Mathias Walukagga asema hatoacha siasa

Amesema bado amejitolea katika siasa na anapanga kurejea kuwania nafasi ya uongozi mwaka 2031.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji wa Uganda Mathias Walukagga amesema hataacha siasa licha ya kukosa ubunge wa Busiro Mashariki baada ya uteuzi wake kuzuiwa kutokana na masharti ya sifa za kielimu.

Akizungumzia matukio yaliyotangulia uchaguzi mkuu wa mwaka 2026, Walukagga alidai kuwa kugombea kwake kulikwamishwa bila haki kupitia njama za kisiasa zilizohusisha aliyekuwa Spika wa Bunge Anita Among, aliyekuwa Mbunge wa Busiro Mashariki Medard Sseggona na maslahi mengine ya kisiasa.

“Nilihuzunika sana na nikakasirika kwa sababu niliamini nilistahili kupatiwa tiketi ya NUP. Walifikiri kuniondoa kungewarahisishia wengine kushinda,” alisema Walukagga.

Walukagga alidai kuwa waliopinga uteuzi wake walitarajia aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Medard Sseggona, angebaki na kiti hicho bila changamoto.

Hata hivyo, alisema Emmanuel Magoola ndiye alichaguliwa mbunge wa eneo hilo, jambo analoamini lilionyesha kuwa mkakati huo haukufanikiwa.

Licha ya changamoto hiyo, mwanamuziki huyo mkongwe amesema bado amejitolea katika siasa na anapanga kurejea kuwania nafasi ya uongozi mwaka 2031.

Kwa sasa, Walukagga amesema anaelekeza nguvu zake katika taaluma yake ya muziki huku akiendelea kujiandaa kwa jaribio jingine la kuwania nafasi ya kisiasa siku zijazo.

Share This Article