Watu 22 wafariki kwenye ajali ya kuporomoka kwa mgodi Tanzania

Marion Bosire
2 Min Read

Watu 22 wamethibitishwa kufariki kwenye ajali ya kuporomoka kwa mgodi katika eneo la kaskazini mwa taifa jirani la Tanzania, kulingana na serikali ya nchi hiyo.

Ajali hiyo ilitokea katika mgodi wa Ng’alita ulioko katika wilaya ya Bariadi katika mkoa wa Simiyu kulingana na taarifa ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Rais Samia alisema, “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 21 kufuatia ajali ya kufunikwa na ardhi katika Mgodi wa Ng’alita, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu. Ndugu zetu hawa walikuwa wachimbaji wadogo katika eneo hili, wakijitafutia riziki zao, familia zao na kuchangia maendeleo ya taifa letu.”

Aliendelea kwa kutuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu hao waliofariki huku akisema maafisa wa usalama walikuwa wakijibidiisha kutafuta miili kwenye vifusi vya mgodi huo.

Kaimu kamanda wa eneo hilo alitangaza mwisho wa operesheni ya kutafuta miili katika mgodi huo jana jioni akiongeza kwamba wote waliofariki walikuwa wanaume.

Watu hao wanasemekana kukaidi agizo la kutotekeleza shughuli za uchimbaji kwenye migodi lililotolewa na wasimamizi wa eneo hilo kwa sababu ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Mvua hiyo kubwa imekuwa ikisababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko katika eneo hilo.

Share This Article