Sikukuu ya Pasaka iligeuka kuwa tanzia katika kaunti ya Makueni jana Jumatatu baada ya watu 10 kufariki katika ajali ya barabarani katika eneo la Salama kwenye barabara kuu ya Nairobi – Mombasa.
Watu wengine 11 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyohusisha magari kadhaa saa mbili na nusu usiku.
Uchunguzi wa awali ulidokeza kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori lililokuwa limebeba mchanga kupoteza mwelekeo na kuyagonga magari matatu yaliyokuwa yamefuatana ana kwa ana.
Kulingana na ripoti ya polisi, abiria tisa walifariki papo hapo huku mtoto mmoja akitangazwa kuwa amefariki baada ya kufikishwa katika hospitali ya Sultan Hamud.
Msimamizi wa matibabu katika hospitali hiyo Dkt. Jane Mwende alisema walisajili miili 10 na majeruhi 11 kutoka kwa ajali hiyo.
“Tulipokea miili tisa kutoka kwa ajali hiyo iliyojumuisha wanaume wanne, wanawake watatu na watoto wawili. Hata hivyo, mtoto mmoja alifariki akiwa hospitalini tulipokuwa tukiwahudumia majeruhi 11, ambapo wengi wao walikuwa na majeraha ya kichwa na kuvunjika kwa sehemu za mwili,” alisema Dkt. Mwende.
Aidha alidokeza kuwa wagonjwa sita wamehamishiwa hospitali ya Makindu kwa matibabu maalum huku watatu wakichukuliwa na jamaa wao na kupelekwa katika hospitali moja ya Nakuru.