Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki amewataka maafisa wote wanaohusika na utekelezaji wa sheria kote nchini, kuunda mpango wa kuhakikisha sheria za trafiki zinafuatwa.
Kindiki aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa afisi za naibu kamishna wa kaunti katika eneo la Kisumu Magharibi leo, alisema lengo la mpango huo wa utekelezaji wa sheria za trafiki ni kukomesha ajali zinazoshuhudiwa kila siku nchini.
Mpango huo alisema utatekelezwa kwa ushirikiano wa idara ya trafiki katika huduma ya taifa ya polisi na shirika la uchukuzi na usalama barabarani NTSA.
Watendakazi wa idara hizo mbili watahakikisha kuondolewa kwa magari mabovu barabarani, kukamatwa kwa wanaovunja sheria za trafiki wakiwemo madereva na wanaotembea kwa miguu na kuhakikisha sheria za trafiki zinafuatwa.
Waziri Kindiki alionya kwamba afisa yeyote wa utekelezaji sheria atakayepatikana akijihusisha na ufisadi barabarani au kwingine atachukuliwa hatua kali kisheria.
Haya yanajiri wakati ambapo ajali nyingi zimekuwa zikiripotiwa sehemu mbali mbali nchini ikiwemo ya jana jioni ambayo ilihusisha basi la chuo kikuu cha Kenyatta na Lori katika eneo la Maungu, barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Mombasa.
Wanafunzi 11 wa chuo hicho walifariki huku wengine 46 wakiachwa na majeraha mabaya.