Trump kuiwekea Urusi vikwazo na ushuru mpya

Martin Mwanje & BBC
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anafikiria kuiwekea Urusi vikwazo na ushuru mpya kufuatia mashambulizi makali ya usiku dhidi ya Ukraine.

Trump aliandika: “Kutokana na ukweli kwamba Urusi inashambulia kwa nguvu Ukraine hivi sasa, ninazingatia kwa nguvu vikwazo vikubwa vya kibenki na ushuru dhidi ya Urusi hadi mapatano ya kusitisha vita na makubaliano ya mwisho ya amani yatakapofikiwa. Kwa Urusi na Ukraine, nendeni kwenye meza ya majadiliano sasa, kabla hamjachelewa!!Asanteni”.

Ujumbe wa hivi karibuni kutoka kwa Trump kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social unazungumzia “shambulio kubwa” ambalo limelenga Ukraine, akimzungumzia Urusi baada ya mashambulizi ya usiku yaliyoathiri maeneo ya makazi na miundombinu muhimu ya nishati.

Katika mji wa bandari wa Odesa, serikali ya mkoa imesema kwamba kulikuwa na milipuko kadhaa ya moto, huku wafanyakazi wa zimamoto wakikimbilia kwenye eneo la tukio.

Kabla ya Rais wa Marekani kuitahadharisha Urusi kuhusu vikwazo zaidi ili kulazimisha makubaliano ya amani, alikuwa akielekeza shinikizo kwa Ukraine.

Mwanzo wa juma hili, Ikulu ya Marekani ilisema kuwa nchi hiyo itasitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine kwa muda huku ikiangalia kama msaada huo unachangia kwenye suluhisho la mgogoro.

Machi 4 mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema kwamba Rais alikuwa akishughulikia “kuwaleta Warusi kwenye meza ya majadiliano”.

Siku moja baadaye, Marekani ilitangaza kuwa itasitisha kushirikiana kwa taarifa za kijasusi na Ukraine.

Mshauri wa Usalama wa Marekani, Mike Waltz, alisema wakati huo kuwa utawala wa Trump ulikuwa ukisitisha na kupitia “vipengele vyote vya uhusiano huu.”

Martin Mwanje & BBC
+ posts
Share This Article