Watanzania waadhimisha siku ya Nyerere

Marion Bosire
1 Min Read
Rais Samia katika ibada ya kumkumbuka Nyerere

Siku ya kumkumbuka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere huadhimishwa Oktoba 14 kila mwaka kulingana na kalenda ya nchi ya Tanzania.

Mwaka huu haikua tofauti na ibada ya kumkumbuka Rais huyo wa kwanza wa taifa jirani la Tanzania iliandaliwa katika Parokia ya Roho Mtakatifu, Babati Mjini, Jimbo Katoliki la Mbulu.

Kupitia mitandao ya kijamii Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alihudhuria ibada hiyo alisema kwamba miaka 24 tangu kifo cha Nyerere bado wanajivunia misingi aliyojenga Nyerere ambaye alimrejelea kuwa mmoja wa waanzilishi wa taifa la Tanzania.

“Tunajivunia misingi aliyotujengea, inayoendelea kutufanya kubaki Taifa moja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo kila mmoja katika nchi yetu ana jukumu la kuendelea kuitunza, kuilinda na kuisimamia.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye ujumbe wa Rais Samia.

Nyerere aliongoza nchi ya Afrika mashariki iliyofahamika wakati huo kama Tanganyika kwanza kama waziri mkuu kati ya mwaka 1961 na 1962 na baadaye kama Rais mwaka 1962 hadi 1964.

Ilipobadilika na kuwa Tanzania aliiongoza hadi mwaka 1985. Yeye ndiye mwanzilishi na mwenyekiti wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho baadaye kilibadili jina na kuwa Chama cha Mapinduzi CCM, ambacho kinaongoza Tanzania hadi sasa.

Aliaga dunia Oktoba 14, 1999 huko London Uingereza.

Share This Article