Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kimezuiwa kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi nchini humo – INEC ilitangaza uamuzi huu jana Jumamosi ikielezea kwamba chama hicho kilikosa kutia saini makubaliano ya lazima ya kanuni za maadili kulingana na makataa ya uchaguzi huo.
Mkurugenzi wa uchaguzi katika tume hiyo Ramadhani kailima alisema kwamba chama chochote ambacho hakikutia saini makubaliano hayo hakitakubaliwa kushiriki uchaguzi mkuu na kwamba mafuruku hiyo ni mpaka mwaka 2030.
Tangazo hilo linajiri siku chache baada ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu kushtakiwa kwa uhaini akilaumiwa kwa kuchochea uasi na kujaribu kuzuia kuendelea kwa mchakato wa uchaguzi.
Waendesha mashtaka walidai kwamba Lissu alihimiza umma kuchukua hatua dhidi ya shughuli ya kupiga kura lakini hakukubaliwa kuwasilisha ombi lolote katika shtaka hilo ambalo adhabu yake inajumuisha hukumu ya kifo.
Mwaniaji huyo wa awali wa Urais amekuwa akikosoa serikali ya Tanzania ya chama cha CCM na kiongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anawania muhula wa pili afisini.
Awali chama cha CHADEMA kilitishia kususia uchaguzi iwapo mageuzi faafu hayangetekelezwa katika mfumo wa uchaguzi.
Mapema jana chama hicho kilithibitisha kwamba kingehudhuria hafla ya kutia saini makubaliano ya lazima ya kanuni za maadili kikisema ni sehemu ya mpango wake mpana wa kushinikiza mageuzi katika namna uchaguzi unaendeshwa.
Kuondolewa kwa CHADEMA kwenye uchaguzi na kushtakiwa kwa kiongozi wake kwa uhaini, vinatarajiwa kuzua maswali kuhusu hali ya demokrasia nchini Tanzania.