Angaa watu watano waliripotiwa kufariki katika ajali iliyotokea katika eneo la Athi River, kaunti ya Machakos,barabara kuu ya Nairobi-Mombasa Jumatano usiku .
Kulingana na ripoti ya Polisi ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa moja na dakika 40 usiku, ikihusisha gari la Matatu la chama cha Kinatwa na lori la Isuzu.
Shahidi alisema Matatu hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Mombasa kuelekea Nairobi, wakati dereva alipojaribu kuyapita magari mengine kiholela na ikakutana uso kwa uso na lori.
Walioaga dunia papo hapo ni pamoja na dereva wa Matatu na abiria wake wanne, huku Polisi wakisema kuwa abiria wengine saba walipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya Machakos Level Five Hospital wanapopokea matibabu.