Maafisa wa polisi leo Jumatatu wameshika doria katika maeneo mengi humu nchini ili kukabiliana na waandamanaji waliojihusisha katika visa vya uharibifu wa mali.
Katika maeneo kadhaa kama vile mjini Ruiru, Kangemi na Kitengela, waandamanaji wa kupinga kuongezwa kwa bei ya mafuta wameonekana wakifunga barabara, kuwasha moto pamoja na kuwavamia waenda kwa miguu na magari ya kibinafsi.
Mgomo huo wa kitaifa unapinga kuongezwa kwa bei ya mafuta na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA), wiki iliyopita.
Katikati ya jiji la Nairobi, takriban maduka yote yalisalia yamefungwa huku wafanyabiashara wakihofia kuporwa.
Idara ya Polisi imesema imechukua tahadahri na kuahidi kutoa usalama wa kutosha kote nchini wakati wa maandamano hayo.