Washukiwa wawili wa wizi wamekamatwa na maafisa wa kitengo cha Upelelezi wa Jinai, DCI huko Lessos karibu na mji wa Kitale kaunti ya Trans Nzoia.
Maafisa hao walipata simu za rununu zinazoshukiwa kuibwa kufuatia operesheni iliyoendeshwa kwa misingi ya taarifa za kijasusi walizopokea katika eneo la Lessos.
Maafisa kutoka Kitengo cha Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi,CRIB kwa ushirikiano na maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Matisi, walivamia makazi karibu na Kanisa la Airport katika Lessos.
Operesheni hiyo ilisababisha kukamatwa kwa Silas Wanjala wa umri wa miaka 24 na Job Kiberenge Sikuku wa miaka 28, ambao bado wanazuiliwa.
Jumla ya simu za rununu 213 za miundo mbalimbali zilipatikana, pamoja na mashine ya Pandora inayoshukiwa kutumika katika kurekebisha upya programu za simu na kompyuta mpakato tatu aina ya HP.
Vifaa vyote vimehifadhiwa kama ushahidi vikisubiri uchunguzi wa kitaalamu wa kisayansi.
Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha vifaa hivyo na kuwatambua washirika wengine wa mtandao huo. Washukiwa watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.