Washukiwa wawili wa ujambazi wakamatwa Dandora

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wawili wa ujambazi wakamatwa Dandora.

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoka kituo cha polisi cha Dandora, wamewakamata washukiwa wawili kwa madai ya kuhusika katika wizi na ubakaji.

Wawili hao Ben Waimari na Moses Odhiambo almaarufu Pascal, ambao wanazuiliwa na maafisa wa polisi, wanadaiwa kutekeleza makosa hayo Machi 11, 2025.

Kulingana na DCI, mwathiriwa alikuwa akiendesha gari lake kwenye barabara ya Ruai-Kangundo akielekea nyumbani, kabla ya gari lake kukwama kwenye tope.

Akiwa katika juhudi za kukwamua gari lake, Waimari, Odhiambo na wengine watano walijitokeza wakisingizia kumsaidia. Hata hivyo baada ya gari kuondoka kwenye tope, washukiwa hao walimfunga katika upande wa nyuma wa gari na wakaliendesha hadi katika mtaa wa Dandora.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema washukiwa hao walimwibia na kumbaka mshukiwa huyo, lakini kamsa za mwathiriwa ziliwavutia waendeshaji wengine wa magari waliofika kumsaidia huku wahalifu hao wakitoroka.

Mwathiriwa alipelekwa hospitalini kwa matibabu, tukio hilo likiripotiwa katika kituo cha polisi cha Kwa Mbao.

Kufuatia uchunguzi wa kina, maafisa wa polisi waliwasaka washukiwa hao na kuwatia mbaroni wawili kati yao, ambao waliwapeleka polisi katika mtaa wa Maringo na Buruburu ambako gari la mwathiriwa lilipatikana.

Washukiwa hao wanahojiwa na maafisa wa polisi, huku msako dhidi ya washirika wao ukiendelea.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article