Washukiwa watatu wakamatwa kwa kumdhulumu mwanamke Nyamira

Tom Mathinji
2 Min Read
Watu watatu wakamatwa kwa kumdhulumu mwanamke Kisii.

Washukiwa watatu wametiwa mbaroni katika eneo la Nyabisimba kaunti ya Nyamira, kwa madai ya kumdhulumu mwanamke kwenye hafla ya mazishi.

Watatu hao Robert Pokea Sarudi mwenye umri wa miaka 43, Bismark Ondiek Sarudi mwenye umri wa miaka 40 na Lameck Ogindo Osoro mwenye umri wa miaka 27, wanadaiwa kumlazimisha mwanamke huyo kushiriki tambiko la kitamaduni kinyume na mapenzi yake, na hivyo kumdhulumu na kusababisha majera kwenye mwili wake.

Kisa hicho kilitokea Machi 21, 2025, wakati mwanamke huyo aliyekuwa ameolewa kwa muda wa miaka tisa na mume wake ambaye sasa ni marehemu, alijipata katika mzozo wa kifamilia.

Baada ya kutalikiana na mume wake, alifahamishwa kuhusu kifo cha baba huyo wa watoto wake na kuarifiwa awapeleke watoto wamzike baba yao, aliyefariki kupitia ajali ya barabarani.

Wakati wa mazishi, baadhi ya jamaa wa mwendazake walimlazimisha mwanamke huyo kushiriki tambiko la kitamaduni la kurusha mchanga kwenye kaburi, lakini alikaidi na hapo akaanza kushambuliwa akilaumiwa kwa kusababisha kifo cha mume wake.

Maafisa wa usalama walifahamishwa kuhusu kisa hicho na polisi wakaanza uchunguzi mara moja, na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa hao watatu katika eneo la Mwongorisi.

Kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiambere, wakisubiri kufunguliwa mashtaka mahakamani.

kulingana na Idara ya DCI kupitia ukurasa wa X, juhudi zinaendelea kuwasaka na kuwashtaki washukiwa zaidi wanaodaiwa kuhusika katika kisa hicho.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article