Maafisa wa polisi kaunti ya Mombasa, wamewakamata washukiwa watatu wa ujambazi, wanaodaiwa kupanga visa vya uhalifu katika eneo hilo.
Kupitia mtandao wa X, idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, ilisema ilipata habari za kijasusi na kuvamia maficho ya wahalifu hao katika mtaa wa Nyali, na kuwakamata washukiwa wawili Ali Ahmad Ali almaarufu “Mkali,” na Abdulrahman Arafat.
Baada ya kuhojiwa, wawili hao waliwaongoza maafisa wa polisi hadi katika nyumba yao ya kukodisha karibu na shule ya upili ya Allidina Visram, ambapo maafisa wa polisi walimkamata mshukiwa wa tatu Mohamed Zulf.
Katika nyumba hiyo, maafisa hao walipata panga nne, vyuma viwili aina ya Y-6 vilivyonolewa pande mbili, misokoto 18 ya bangi, aina 10 za simu zinazoshukiwa kuibwa, mifugo wanne, runinga na mtungi wa gesi ya kupikia.
Kulingana na maafisa hao wa DCI, washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa, wakisubiri kufikishwa mahakamani.