Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Mombasa

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wa Mihadarati wakamatwa mombasa.

Maafisa wa asasi mbali mbali za usalama wamewakamata washukiwa watatu wa ulanguzi wa mihadarati katika eneo la likoni kaunti ya Mombasa.

Maafisa hao kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kitengo cha Kukabiliana na mihadarati (ANU), Halmashauri ya Taifa dhidi ya Pombe na dawa za kulevya (NACADA), na Maafisa wa Ukusanyaji Ushuru (KRA), walitekeleza operesheni hiyo wakilenga walanguzi hao wa mihadarati baada ya kupashwa habari na wananchi.

Washukiwa hao Johnson Onderi, Felista Ratemo na Margret Wanjiku, walinaswa katika nyumba moja  mtaa wa Corner Mpya,  Likoni, wakipakia kile kinachoaminika kuwa pombe iliyokuwa na nembo  SMART Vodka.

Aidha kwenye msako huo, maafisa hao pia walipata vibandiko bandia vya Halmashauri ya ukusanyaji Ushuru KRA.

Maafisa hao kisha walifululiza hadi katika eneo la  Shika Adabu, ambako waliwatia nguvuni Charles Onderi na Hezron Migiro ambao walipatikana na kile kilichoaminika kuwa dawa ya kulevya aina ya heroine yenye thamani ya shilingi 4,600,000.

Share This Article