Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), ameidhinisha mashtaka ya ugaidi dhidi ya washukiwa 37, waliofikishwa kwenye mahakama ya Kahawa.
Mashtaka hayo yaliidhinishwa baada ya washukiwa hao kutiwa nguvuni katika kaunti za Kiambu na Machakos.
Kulingana na taarifa ya DPP, miongoni mwa waliofikishwa mahakamani, ni washukiwa 25 wanaodaiwa kutekeleza makosa ya ugaidi Juni 25, 2025 kati ya saa sita mchana na saa tano usiku.
“Wanadaiwa kuharibu vifaa vya serikali, vinavyojumuisha Mahakama ya kikuyu, Afisi za kaunti ndogo ya kikuyu, afisi ya chifu kikuyu, afisi ya usajili wa watu kikuyu, afisi ya kaunti ndogo ya elimu, afisi ya usajili wa ardhi, kituo kidogo cha polisi cha Dagoretti na afisi ya naibu kamishna wa kaunti ya kikuyu,’ilisema taarifa hiyo.
Vile vile, DPP alidokeza kuwa washukiwa hao wanakabiliwa na kosa tofauti la uteketezaji, na shtaka mbadala la uharibifu wa mali.
Washukiwa hao walifikishwa mahakamani pamoja na Peter Kinyanjui Wanjiru, almaarufu Kawanjiru, na Serah Wanjiku Thiga, ambao wanakabiliwa na mashtaka sawa na hayo.
DPP pia aliidhinisha mashtaka dhidi ya ugaidi kwa watu 10 waliokamatwa Matuu kaunti ya Machakos.
Wanadaiwa kutekeleza makosa hayo Juni 25,2025 katika kituo cha polisi cha Matuu, na kusababisha uharibifu wa vifaa vya serikali ikiwa ni pamoja na magari ya polisi na kuwadhulumu maafisa wa polisi waliokuwa zamuni.