Mitambo 31 ya bayogesi yazinduliwa kaunti ya Nyandarua

Hadi sasa, miradi yenye thamani ya zaidi ya KSh. 136 milioni inaendelea kutekelezwa katika wadi zote 25 za Kaunti ya Nyandarua.

Lydia Mwangi
3 Min Read

Utekelezaji wa Mpango wa ufadhili wa hatua za Kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi zinazoongozwa na Jamii (FLLoCA) katika Kaunti ya Nyandarua unaendelea kushika kasi, huku mitambo 31 mipya ya bayogesi ikizinduliwa leo katika Wadi ya Gathanji.

Mradi huu unaongozwa na Gavana Dkt. Moses Kiarie Badilisha unalenga kulinda Msitu wa Kwa Ng’ara ambao ni eneo nyeti kimazingira dhidi ya ukataji miti kiholela, sambamba na kukuza matumizi ya nishati safi kwa jamii za eneo hilo.

Mpango wa FLLoCA ni ushirikiano kati ya Serikali ya kitaifa, Serikali za Kaunti, Benki ya Dunia, na wadau wengine wa maendeleo.

Unalenga suluhu endelevu zinazoongozwa na jamii, ukitumia rasilimali zilizopo ndani ya maeneo husika na maarifa asilia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mitambo hiyo ya biogesi, Gavana Badilisha alisisitiza dhamira ya serikali yake ni kuendeleza miradi ya nishati safi inayowezesha wananchi na kulinda rasilimali za asili.

“Uzinduzi wa leo ni hatua nyingine muhimu katika azma yetu ya kulinda misitu yetu na kutoa mbadala endelevu kwa wananchi. Mitambo hii ya biogesi haitatunza tu mazingira bali pia itaboresha maisha ya watu wetu,” alisema Gavana.

Mmoja wa walionufaika, Bi Tabitha Wanjiru, akizungumza kutoka nyumbani kwake, alisifu mpango huu kwa kubadilisha maisha yake ya kila siku.

“Sihitaji tena kutembea umbali mrefu kutafuta kuni. Mtambo huu wa biogesi umenipunguzia mzigo na kuokoa msitu wetu,” alisema.

Shule ya Sekondari ya Gathanji pia imenufaika na mradi huu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo alieleza kuwa mradi wa biogesi umepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni na kuboresha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi.

“Akiba tuliyopata kwenye bajeti ya kuni imetuwezesha kuelekeza rasilimali zaidi kwenye mahitaji ya kielimu. Wanafunzi wetu sasa wanasoma katika mazingira safi na yenye afya,” alieleza mwalimu mkuu.

Hadi sasa, miradi yenye thamani ya zaidi ya KSh. 136 milioni inaendelea kutekelezwa katika wadi zote 25 za Kaunti ya Nyandarua.

Miradi ya nishati safi kama vile mitambo ya biogesi imelenga zaidi wadi zinazoizunguka misituambayo ni vyanzo muhimu vya kaboni vinavyokabiliwa na hatari kutokana na uvunaji wa kuni usiodhibitiwa.

Kwa sasa, mitambo 62 ya biogesi inayosaidia zaidi ya kaya 300 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika Wadi ya Gathanji na maeneo jirani.

Serikali ya kaunti inalenga kupanua juhudi hizi ili kuhakikisha uendelevu wa mazingira na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wakazi.

Mpango wa FLLoCA unathibitisha nguvu ya hatua zinazoongozwa na jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani huku ukihakikisha ustawi wa maisha ya watu mashinani.

Lydia Mwangi
+ posts
Share This Article