Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania, BASATA, Edward Buganga, amewataka wasanii na wadau wa sanaa kuwa mabalozi wema.
Kulingana na Buganga, wasanii wanafaa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali, huku wakitumia ushawishi wao katika jamii kuwa mabalozi wema kupitia kazi zao.
Buganga alisema hayo jana Agosti 31, 2026, katika mkutano wa mafunzo kuhusu Ulinzi wa Sarafu kwa Wasanii yaliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na BASATA.
Mafunzo hayo yalishirikisha wasanii zaidi ya 150 kutoka fani mbalimbali, zikiwemo Muziki, Filamu, Ufundi na Sanaa za Maonyesho.
Amesisitiza kuwa wasanii wana ushawishi mkubwa na wanafuatiliwa na watu wengi, hivyo wanapaswa kutumia nafasi hiyo kutoa ujumbe unaojenga, kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu masuala muhimu ya Taifa, ikiwemo umuhimu wa kulinda sarafu.
Aidha, amewataka wasanii kushirikiana na Serikali na taasisi zake katika kutoa elimu kwa wananchi kwa kutumia ubunifu wa sanaa.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, yalilenga kuongeza uelewa wa wasanii kuhusu ulinzi wa sarafu na masuala ya fedha.