Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya Peterson Ngetha Githinji, maarufu kama Pitson ametoa ushuhuda kuhusu watoto wake mbele ya kanisa katika hatua inayovutia hisia kali.
Pitson ambaye pia ni mhubiri, ameonekana kwenye video moja iliyonakiliwa kanisani akiwa amesimama mbele na mkewe na wanawe.
Anasikika akitoa ushuhuda kuhusu jinsi familia yake imepitia changamoto kuhusiana na afya ya watoto lakini mwishowe alipata kuzishinda changamoto hizo.
Mwanawe wa kwanza wa kike, Pitson alisema alizaliwa na tatizo la miguu iliyopinda wakampeleka hospitali ambapo alihudumiwa na sasa miguu yake imenyooka.
“Ndoto yake atakapokuwa mtu mzima ni kuwa mcheza densi,” alisema Pitson huku akisonga mbele na kuzungumzia mwanawe wa pili.
Mtoto huyo wa pili naye, alichelewa kuongea hatua aliyoafikia akiwa na umri wa miaka mitano. Pitson alimpa nafasi ya kusalimia waumini kama njia ya kudhibitsha kwamba yuko sawa sasa.
Kitindamimba wao ambaye ni wa kiume naye alizaliwa akiwa na rangi mbili tofauti usoni, ambapo upande mmoja alikuwa mweupe na nusu nyingne ya uso ikawa nyeusi.
Rangi ya mtoto huyo ilibadilika na kuwa moja kadri alivyokua babake akisema kwamba hawakumlea na wasiwasi kwani madaktari waliwahakikishia kwamba alikuwa sawa kabisa alipozaliwa.
Pitson alipata umaarufu mwaka 2014 kutokana na wimbo wake “Lingala Ya Yesu” na tangu wakati huo amejibidiisha kiasi cha kuorodheshwa miongoni mwa wasanii bora wa nyimbo za injili nchini.
Mwimbaji huyo aliwekwa wakfu kuhudumu kama mchungaji mwezi Julai 2022, akitangaza hatua hiyo muhimu kwenye mitandao ya kijamii, kupitia video ya sherehe yake ya kuwekwa wakfu.