Mabadiliko ya usimamizi wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, yamefichua mkanganyiko uliopo kuhusu tofauti kati ya mashindano hayo na Miss World Tanzania.
Watumizi wengi wa mitandao walionekana kutofahamu vyema kuhusu tofauti ya Miss Tanzania na Miss World Tanzania na uhalali wa mashindano hayo.
Akizungumza kwenye mahojiano, msimamizi wa mashindano ya Miss World Tanzania Mustafa Hassanal alisema kuwa licha ya kuwa na majina yanayofanana, kila shindano lina malengo na mfumo wake bila kuelezea tofauti zaidi.
Hata hivyo alikubali kwamba mashindano yote kwa pamoja yanakusudia kukuza na kuboresha sekta ya urembo nchini Tanzania.
Kampuni ya The Look nchini Tanzania chini ya uongozi wa Basila Mwanukuzi, ilikabidhi uongozi na uendeshaji wa mashindano ya Miss Tanzania kwa kampuni ya Lamata Village Entertainment ya Leah Richard Mwendamseke.
Huku wengi wa wadau wa sekta ya urembo wakimpongeza Leah wakiamini ataongoza vyema mashindano hayo, wapo ambao wanahisi kwamba bado hajapata uwezo wa kuendesha shindano kubwa kama hilo.
Mwanamitindo Cecilia Godfrey anayeishi Marekani, ambaye amewahi kufanya kazi na watu maarufu kimataifa, anasema anathamini mchango mkubwa wa Lamata katika tasnia ya tamthilia na filamu, lakini anaamini kuwa bado anahitaji muda zaidi kujikita na kuielewa vizuri sekta ya mashindano ya urembo.
Cecilia vile vile alikosoa uwepo wa mashindano mawili tofauti ya urembo nchini Tanzania akihimiza waandalizi waungane shindano liwe moja kwani wanaonyesha picha ya kuchanganyikiwa.