Wanyonyi awarai Wabunge kuwapiga msasa vyema Mawaziri walioteuliwa

Dismas Otuke
2 Min Read

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi amewataka Wabunge kuwapiga msasa ipasavyo Mawaziri walioteuliwa na Rais william Ruto, ili kuhakikisha ni wale tu wanaofaa watakaoidhinishwa.

Wanyonyi amesema pia ipo haja ya kubadilisha mfumo wa kuwapiga msasa Mawaziri, ili kuwapa wananchi fursa ya kufanya uamuzi kuhusu wanaopendekezwa kuongoza wizara.

“Itakuwa vizuri tubadilishe sheria ili raia wapate fursa ya kutoa maoni na kuwapiga msasa Mawaziri wanapoteuliwa badala ya hali ya sasa ambapo kamati ya bunge huwatathmini kabla ya kuwasilisha majina bungeni na hatimaye kwa Rais kwa uteuzi.”akasema Wanyonyi

Mbunge huyo pia ametaja malumbano yanayoendelea katika muungano wa Azimio la Umoja kuwa hali ya kawaida katika chama au muungano wowote  wenye Demokrasia.

Hata hivyo Mbunge huyo wa chama cha Orange Democratic Movement(ODM) amesema malumbano hayo yanasababishwa na ubinafsi miongoni mwa wamachama wa Azimio.

“Hiyo ni kawaida ya Demokrasia ila sababu kubwa ya malumbano hayo ni ubinafsi kuna watu ambao wameweka maslahi yao mbele, badala ya taifa au chama.”akaongeza Wanyonyi

Mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa tatu amewapongeza vijana wa Gen Z kwa kujitokeza na kuangazia utawala na usimamizi wa taifa lao.

“Vijana wetu wa Gen Z wamefanya jambo zuri sana na kila nchini inaangazia Kenya,na hii tu ndio njia ya kuhakikisha viongozi wanawajibika ipasavyo ninawapongeza.”akasema Wanyonyi

Website |  + posts
Share This Article