Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi ametoa hakikisho kwamba kuna akiba ya kutosha ya mafuta nchini.
Hata hivyo, Wandayi amekosa kuelezea akiba hiyo inaweza ikadumu kwa muda gani.
Kumekuwa na madai kwamba akiba ya mafuta iliyopo nchini inaweza ikadumu kwa takriban wiki tatu.
Waziri Wandayi alitoa hakikisho hilo wakati kukiwa na hofu ya kuwepo uhaba wa mafuta kutokana na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
Akiwahutubia wanahabari leo Jumatano, Wandayi amezionya kampuni za mafuta dhidi ya kuhodhi bidhaa hiyo akitaja hatua hiyo kuwa ukiukaji wa sheria.
Huku uhaba wa bidhaa hiyo ukitazamiwa, baadhi ya kampuni zimeripotiwa kuhodhi mafuta zikitazamia bei yake itapanda hivi karibuni kabla ya kuyauza.
“Tunaweza tukathibitisha ripoti za kuhodhi mafuta kwa kutazamia mabadiliko ya bei,” alisema Waziri Wandayi.
“Tunataka kuzikumbusha kampuni za mafuta juu ya majukumu yao ya kikatiba la sivyo zichukuliwe hatua.”
Wizara inasema miongoni mwa hatua ambazo kampuni hizo zitachukuliwa ni kupokonywa leseni.
Taarifa hii imechangiwa na mwandishi wetu Regina Manyara