Wandayi: Bei za umeme hazitaongezwa

Waziri huyo alidokeza kuwa mabadiliko ya bei za umeme katika siku za usoni ni sharti yazingatie sheria.

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Nishati na Petroli Opiyo Wandayi.

Waziri wa Nishati na Petroli Opiyo Wandayi amethibitisha kuwa bei za umeme hazitaongezwa, baada ya ombi lililowasilishwa kufanyia mabadiliko bei hizo kuondolewa.

Hatua hiyo inawapa Wakenya afueni, kwa kuwa sasa wataendelea kulipa bei za umeme zilizopo.

Wandayi alisema ombi hilo ambalo lilikuwa limewasilishwa na kampuni ya usambazaji umeme ya Kenya power, limeondolewa baada ya mashauriano ndani ya serikali na wadau katika sekta ya nishati.

Kwenye mkutano na wanahabari leo Jumatano, Wandayi alisema hatua hiyo inalenga kukinga biashara, nyumba na viwanda dhidi ya gharama za juu za umeme, huku ikipiga jeki ukuaji wa kiuchumi na kubuni nafasi za ajira.

“Kufuatia kuondolewa kwa ombi hilo, bei ya sasa ya umeme itasalia jinsi ilivyo, hadi itakapotangazwa tena kuambatana na sheria ya nishati na taratibu za udhibiti,” alisema Wandayi.

Waziri huyo alidokeza kuwa mabadiliko ya bei za umeme katika siku za usoni ni sharti yazingatie sheria ikiwa ni pamoja na ukadiriaji wa kiufundi, ushiriki wa wadau na ule wa umma.

TAGGED:
Share This Article