Wanawake wamehimizwa wawanie nyadhifa za uongozi kwa wingi, mkakati utakaowahakikishia uwakilishi katika bunge la taifa, Seneti na mabunge ya kaunti.
Wabunge wa kike walikongamana mjini Machakos kumotisha wanawake wanaopania kuwa viongozi katika kikao kilichoandaliwa na chama cha wanwake wa sekta ya elimu FAWE.
Waliwataka wanawake wajitahidi kuelewa mienendo ya siasa na sababu zinazowachochea kuingilia sasa.
Kiranja wa wachache bungeni Milly Odhiambo alisema kwamba siasa za Kenya zimetawaliwa na wanaume na imekuwa changamoto kubwa kwa wanawake wanaotaka kuwa viongozi lakini akawahimiza kusalia macho na kutokata tamaa.
Odhiambo alipongeza kizazi cha Gen Zs kwa maandamano walioyoandaa hivi maajuzi akisema yamewapa funzo muhimu kwamba enzi ya kujionyesha na mali yao imeisha.
Beatrice Elachi kwa upande wake anaamini kwamba mtazamo wa jamii kuhusu wanawake umekuwa kikwazo cha muda mrefu katika kujihusisha na siasa.
Mbunge huyo wa eneo la Dagoretti Kaskazini anahisi kwamba ushauri kwa wanawake wanaowania uongozi utawapa uwezo wa kushinda vikwazo na kuafikia ufanisi.
Elachi aligusia masuala kama mavazi na mwonekano ambayo alisema ni muhimu na kwamba wapo walioafikia ufanisi huku wengine wakikosa kuuafikia kutokana na masuala kama hayo tu.
Msimamizi wa mawasiliano kwenye FAWE barani Afrika Kossi Tsenou alitahadharisha wanawake wanaotaka kuingilia siasa kuwa macho kwa uchaguzi wa mwaka 2027 na kufahamu changamoto zinazotarajiwa.