Wanasheria wakosoa matamshi ya Rais kuhusu idara ya mahakama

KBC Digital
2 Min Read
Erick Theuri, Rais wa chama cha LSK

Chama cha wanasheria nchini, LSK kimeonyesha kutoridhishwa kwake na matamshi ya kiongozi wa nchi kuhusu mahakama. Kwa sababu hiyo, wanachama wote wa chama hicho kote nchini wamehimizwa kuvaa tepe za rangi ya zambarau na kujiunga na maandamano ya amani.

Kwenye taarifa iliyotiwa saini na rais wa chama cha LSK Eric Theuri, chama hicho kinasema kwamba katiba ya Kenya ya mwaka 2010 iliondoa ukuu na mamlaka ya kipekee katika bunge na kupatia kila tawi la serikali nguvu zake kulingana na matakwa ya Wakenya.

“Uwezo huo unaweza tu kutumiwa kwa mujibu wa katiba,” aliandika Theuri akiongeza kwamba siku za idara ya mahakama kufanywa nambari mbili au kushinikizwa kufanya mambo kwa namna fulani na serikali kuu zimekwisha.

LSK inahimiza Rais kutumia njia mwafaka za kulalamika kuhusu maafisa fulani wa idara ya mahakama ambayo ni kuwasilisha malalamishi kwa tume ya huduma za mahakama, JSC na wala sio kulalamika kwenye mikutano ya hadhara.

Hatua ya Rais ambayo LSK inaitaja kuwa kuchochea umma dhidi ya idara ya mahakama imetajwa na chama hicho cha wanasheria kuwa hatari kwa utiifu wa katiba na kusababisha umma kushuku idara hiyo.

Akizungumza kwenye mazishi ya babake seneta John Methu jana Jumanne, Rais William Ruto alilalamikia kile alichokitaja kuwa hatua ya watu fulani kutumia idara ya mahakama kuhujumu mipango ya serikali.

Mahakama zimekuwa zikitoa maagizo ya kuzuia mambo kadhaa ya serikali yaliyoidhinishwa na bunge kama vile ushuru wa nyumba na sheria ya kifedha ya mwaka 2023 kati ya mengine.

Chama hicho sasa kinamtaka Rais awasilishe ushahidi wowote alionao wa kudhibitisha kwamba maafisa fulani wa mahakama wamehusika kwenye ufisadi kwa tume ya huduma za idara ya mahakama JSC.

LSK imehimiza hulka ya kutii maagizo ya mahakama ambayo ni kipengee muhimu cha katiba ya Kenya ambayo inalenga kuleta mabadiliko.

Chama hicho kimejitolea pia kuhakikisha uhuru wa idara ya mahakama unadumishwa pamoja na uhuru wa afisi nyingine za kikatiba kwa kutekeleza majukumu yao.

KBC Digital
+ posts
Share This Article