Wanafunzi walemavu kupokea mafunzo mitandaoni

Marion Bosire
2 Min Read

Katika mpango wa kihistoria unaolenga kubadilisha sura ya elimu jumuishi nchini Kenya, wanafunzi 850 wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanajiandaa kuanza mafunzo ya mtandaoni ya wiki 14.

Mpango huo wa kipekee unatokana na ushirikiano kati ya wakfu wa Seneta mteule Crystal Asige -CAF na Taasisi ya biashara ya Luxembourg – EBU.

Mafunzo hayo yanazinduliwa rasmi tarehe 15 Septemba 2025, yakitoa kozi zilizoidhinishwa kimataifa katika Usimamizi wa Biashara, Akili Unde kwa Viongozi na Teknolojia na Sayansi ya Data, kwa lengo la kuwapa washiriki ujuzi muhimu kwa ajira za siku za usoni katika ulimwengu unaobadilika kiteknolojia kwa kasi.

“Huu sio mpango tu wa mafunzo – ni ujumbe wa matumaini” alisema Seneta Crystal Asige, mwanzilishi wa CAF na mtetezi maarufu wa haki za watu wenye ulemavu.

“Kwa wengi wao, hii itakuwa mara yao ya kwanza kupata elimu ya kiwango cha kimataifa iliyoandaliwa makhsusi kwa mahitaji yao. Tunavunja minyororo ya kutengwa. Uwezo – sio ulemavu – ndio utakaofungua milango ya fursa.” Aliandika kiongozi huyo.

Hatua hii inajiri wakati muhimu, miezi michache baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2025, inayohakikisha usawa wa upatikanaji wa elimu na ajira.

Mpango wa CAF–EBU umetajwa kuwa kati ya juhudi za mwanzo kutekeleza sheria hiyo kwa vitendo.

EBU imeeleza kujitolea kwake kwa muda mrefu katika ujumuishaji. “Huu ni mwanzo tu,” alisema mwakilishi wa taasisi hiyo.

“Kuanzia 2026, tunatarajia kuwafunza wanafunzi wengine 2,000 wenye ulemavu kila mwaka. Mustakabali ni wa kidijitali — Akili Bandia, Roboti, Blockchain — na hatutaki kumwacha yeyote nyuma.”

Kwa kuwa mafunzo haya yanaendeshwa kwa njia ya mtandaoni, yanavunja vikwazo vya kijiografia na kufungua fursa kwa wanafunzi kutoka maeneo ya mbali kuunganishwa na wakufunzi wa kimataifa na viwango vya mafunzo vya kimataifa.

Wakati Kenya inapoelekea katika uchumi jumuishi na unaoendeshwa na ubunifu, ushirikiano huu unawakilisha zaidi ya utekelezaji wa sheria — ni ishara ya mabadiliko ya kiutamaduni katika kutambua, kukuza, na kuimarisha vipaji.

Website |  + posts
Share This Article