Zaidi ya familia 1,000 zinazoishi karibu na ziwa Naivasha, zinakabiliwa na tisho la kuhamishwa baada ya maji katika ziwa hilo kuongezeka kwa mara ya tatu katika muda wa miaka tano.
Maji hayo kwa sasa yamefurika kwenye makazi na mashamba, na hivyo kuhatarisha kuzuka kwa magonjwa yanayotokana na maji, hasaa baada ya vyoo na vidimbwi kufurika.
Kulingana na mwathiriwa Richard Mwathi, maji hayo yanafurika kila uchao kwenye shule na makazi, huku familia zilizoathiriwa zikilazimika kuhamia mitaa jirani.
“Familia nyingi zinaishi kwenye nyumba zilizofurika kwa kuwa hawana uwezo wa kifedha kuhamia mitaa jirani,” alisema Mwathi.
Akizungumza kwa njia ya simu, waziri wa Afya ya Umma wa kaunti ya Nakuru Joyce Ncece, alisema walitoa tahadhari kwa wanaoishi karibu na ziwa hilo kuhama.
“Hii sio mara ya kwanza kwa viwango vya maji kuongezeka katika ziwa hili. Wale ambao huathiriwa huhama na kurejea maji yanapopungua.