Serikali inatekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa viazi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu zilizoidhinishwa za viazi, katika juhudi za kufanikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini.
Akizungumza Ijumaa katika kaunti ya Nakuru, wakati wa kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Viazi, Katibu wa Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alisema viazi hutekeleza jukumu muhimu katika ukuaji wa uchumi katika maeneo ya mashinani, ikizingatiwa kuwa asilimia 98 ya wanaokuza viazi hapa nchini, ni wakulima wadogo wadogo.
“Ukuzaji viazi ni wa pili hapa nchini baada ya mahindi,na huchangia kuimarisha utoshelevu wa chakula, ukuaji wa uchumi na utoaji nafasi za ajira,” alisema Dkt. Ronoh.
Hata hivyo, katibu huyo alisikitika kuwa uzalishaji viazi hapa nchini ulipungua mwaka 2024 baada ya taifa hili kuzalisha metrik tani Milioni 2.2, kutoka kwa metrik tani Milioni 2.3 mwaka 2023.
“Kiwango cha uzalishaji kilipungua kutoka hekari 239,300 hadi hekari 238,838 katika kipindi hicho,” alifafanua Katibu huyo.
Hata hivyo alielezea umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wote, kuhakikisha sheria za ukuzaji viazi zinazingatiwa.