Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Nyambaria waliojawa na hamaki waliwafurusha wasimamizi wa mtihani wa KCSE jana Alhamisi wakidai kunyanyaswa.
Wanafunzi wa shule hiyo iliyo kaunti ya Nyamira, wamedai kunyanyaswa na haki zao kukiukwa na wasimamizi hao wanapowakagua kabla ya kuanza kwa mtihani huo.
Ilibidi maafisa zaidi wa usalama kutumwa katika shule hiyo ili kutuliza hali.
Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong’o Omogeni amedai wasimamizi wa mtihani huo wamekuwa wakiwafanyia wanafunzi ukaguzi kupitiliza na kumtaka Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kuingilia kati.
Shule ya Upili ya Nyambaria iliongoza katika mtihani wa KCSE mwaka jana na kuibua tuhuma za wizi wa mitihani katika shule hiyo na nyinginezo kutoka eneo la Kisii.