Takriban wanafunzi 40 katika shule moja katika eneo la Kasese magharibi mwa Uganda, wameuawa katika shambulizi la Ijumaa usiku na watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa Allied Democratic Forces.
Wengine wanane katika Shule ya Sekondari ya Lhubiriha, iliyoko chini ya kilomita mbili kutoka mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini, kwa mujibu wa Polisi wa Uganda. Makumi ya wengine wanahofiwa kutekwa nyara.
Polisi wanasema jeshi linawafuatilia wapiganaji hao waliokuwa wamevuka kutoka DRC.
“Ijumaa usiku waasi wa ADF walishambulia shule ya upili ya Lhubiriha iliyoko kilomita mbili kutoka mpaka wa jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo. Hadi kufikia sasa miili 25 imepatikana. Majeruhi wanane pia walipatikana na wanapokea matibabu katika hospitali ya Bwera,” alisema msemaji wa polisi Fred Enanga.
Mwaka jana, vikosi vya usalama vilisema vimewaua makumi ya Wanajeshi wa Allied Democratic Forces (ADF), ambao walikuwa wamevuka Mto Semuliki na kuingia katika wilaya ya Ntoroko nchini Uganda.
Kundi la ADF, kundi la waasi lenye asili ya Uganda ambalo lilikuwa na makao yake katika eneo la Rwenzori katika miaka ya 1990, limekuwa likiendesha shughuli zake kutoka ndani ya DRC likiua, uporaji na utekaji nyara, kwa zaidi ya miongo miwili.
Lakini shambulio dhidi ya shule hiyo ni tukio la kwanza la aina hiyo ndani ya Uganda kwa miaka mingi.
Mnamo 1998, waasi wa ADF walishambulia Taasisi ya Kiufundi ya Kichwamba wilayani Kabarole na kuwachoma moto wanafunzi 80 hadi kufa na kuwateka nyara zaidi ya 100.
Lakini mwaka 2021, kundi hilo la waasi lililaumiwa kwa mfululizo wa mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga nchini Uganda.
Vikosi vya Uganda vilialikwa na serikali ya Kinshasa kwenda mashariki mwa Kongo kupambana na ADF, operesheni ambayo bado inaendelea.