Maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini, EACC leo Jumatano wamewakamata watu watano ambao awali walihudumu katika serikali ya kaunti ya Isiolo kwa tuhuma za ufisadi.
Watano hao ni sehemu ya watu 13 wanaodaiwa kuhusika kwenye ulaghai kupitia manunuzi ya shilingi milioni 58,560,000.
Haya yanahusiana na kandarasi ya kununua na kuwasilisha gari la zima moto iliyotolewa kwa njia isiyofaa kwa kampuni ya Drescoll mwaka wa matumizi ya pesa za serikali wa 2018/2019.
Waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mbele ya mahakama ya kupambana na ufisadi ya Isiolo kesho Alhamisi, Januari 18, 2024.
Wale ambao walikamatwa ni Peter Ngechu Muhuha aliyekuwa afisa mkuu wa masuala ya fedha, Adano Salad Kadubo aliyehudumu kama afisa mkuu wa ujenzi, nyumba na maendeleo ya miji, Abdinassir Ali aliyekuwa akisimamia masuala ya fedha, Jibril Hassan na Augustine Kariuki Gatebu ambao walikuwa wahasibu.