Wito wa Mudavadi kwa Vyuo Vikuu

Martin Mwanje
2 Min Read

Vyuo Vikuu vimetakiwa kukumbatia ubunifu wa kilimo na utafiti ili kubuni suluhisho zitakazopunguza gharama ya maisha.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amesema sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi, ikichangia takriban asilimia 33 ya Pato Ghafi la Taifa, GDP.

Aidha sekta hiyo inaajiri zaidi ya asilimia 40 ya watu wote na asilimia 70 ya watu kutoka sehemu za mashinani.

“Kuna hitaji linaloongezeka la bidhaa za kilimo linalochochewa na ongezeko la idadi ya watu. Kwa mfano, idadi ya watu nchini Kenya inakadiriwa kufikia milioni 55 mwaka huu. Ili kukidhi mahitaji haya yanayoongezeka, ni lazima tuwekeze na kuongeza uzalishaji wa kilimo kila mwaka kwa asilimia isiyopungua mbili,” alisema Mudavadi.

Alisisitiza ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi ya serikali ya Kenya Kwanza inayoangazia utoaji ruzuku kwa uzalishaji badala ya ulaji.

“Ukienda kwa baadhi ya maeneo tulikowapa wakulima fursa kupitia mpango wa mbolea, inaonekana mavuno yatakuwa mazuri. Ina maanisha tumeanza kufanya mambo kuwa sawa.”

Alisema hii ni licha ya hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa ardhi na upungufu wa rasilimali maji.

Aliyasema hayo katika Chuo Kikuu cha Nairobi, UoN wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Tenkonojia na Ubunifu wa Kilimo, ATIC.

Mpango huo unatokana na ushirikiano kati ya UoN na kampuni ya Elgon Kenya Limited.

Mudavadi anasema taasisi ambazo zimejikita kwa sayansi, teknolojia na ubunifu kama ATIC zitaruhusu kutumiwa kwa gharama chache kuongeza uzalishi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *