Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ametangaza kwamba wote ambao walikosa kufanya mtihani wa mwisho wa darasa la nane, KCPE watapata fursa nyingine ya kuufanya Januari, 2024.
Akizungumza katika afisi za Baraza la Mitihani Nchini, KNEC mtaani South C, kaunti ya Nairobi, Machogu alisema Wizara ya Elimu itafanya uchunguzi wa kina kote nchini ili kupata watahiniwa hao.
Kulingana na Waziri, jumla ya watahiniwa 9,354 hawakufanya mtihani wa KCPE wa mwaka 2023.
Alisema watahiniwa hao wataandaliwa mtihani spesheli watakaofanya ili kupata fursa ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Haya yanajiri wakati ambapo mfumo wa elimu unabadilishwa kutoka ule wa awali wa 8.4.4 hadi ule wa umilisi CBC. Na hilo limetimia sasa katika shule za msingi.
Kabla ya kuanza kwa mtihani huo wa darasa la nane KCPE mwaka 2023, serikali ilitoa fursa kwa watahiniwa ambao hawakuwa wamesajiliwa.
Kwa sababu hiyo watahiniwa 205 walijitokeza na hivi leo nao wanapata majibu ya mtihani huo.