Tume ya kuajiri walimu nchini TSC, imesema kwamba ilipokea maombi 314,117 ya kazi kutoka kwa walimu, huku nyadhifa wazi zikiwa elfu 46 pekee.
Nyadhifa hizo zilitangazwa na serikali mwezi huu wa Oktoba.
Mkurugenzi mtendaji wa TSC Nancy Macharia, alizungumza mbele ya Kamati ya bunge kuhusu elimu ambapo alielezea kwamba maombi 93,646 ni ya walimu wa shule za msingi na nafasi zilizotangazwa ni elfu 6.
Maombi mengine 144, 177 alisema ni ya walimu wa shule za sekondari za msingi huku nafasi wazi zikiwa 39,550 pekee.
Nafasi 450 za walimu wa shule za sekondari zinamezewa mate na walimu 76,294.
Tangazo hilo ni sehemu ya uthibitisho wa walimu 46,000 waliohitimu kuajiriwa kwa masharti ya kudumu pamoja na kupata malipo ya kustaafu.
Walimu hao wanatarajiwa kuanza kazi rasmi januari 2025.
Macharia alielezea kwamba TSC inapokea fomu za ajira kutoka kwa afisi zake za kaunti.
Kuhusu kupandishwa vyeo kwa walimu, Macharia alisema tume ilipokea shilingi bilioni moja kutoka kwa wizara ya fedha mwaka wa 2024/2025 ili kutekeleza hilo.