Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa watatu waliokuwa wakisafirisha kilo 196 za bangi, katika eneo la Archers Post, kaunti ya Samburu.
Kulingana na maafisa wa upelelezi wa maswala ya jinai DCI, bangi hiyo iliyokuwa ikisafirishwa na Lori lenye namba za usajili KCZ 198E, ilikuwa imefichwa chini ya Magunia ya maharagwe.
Dereva wa lori hilo Isaack Mohammed Bakacha mwenye umri wa miaka 34 na watu wengine wawili Harun Mohammed Galgalo na Ali Abdikadir Mohammed, walikamatwa na kikosi cha maafisa wa usalama kutoka asasi mbali mbali katika kizuizi cha barabarani.
Bangi hiyo ya thamani ya shilingi milioni 5.9 Kwa sasa inazuiliwa kama ushahidi, huku Lori hilo pia likizuiliwa kusubiri kukamilika kwa uchinguzi.