DRC: Ufaransa yalaani shambulio la ubalozi wake Kinshasa

radiotaifa
2 Min Read
Waandamanaji wakikabiliana na maafisa wa usalama nje ya ubalozi wa Ufaransa mjini Kinshasa / Picha kwa hisani ya Reuters

BBC: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amelaani shambulizi dhidi ya ubalozi wa Ufaransa mjini Kinshasa na waandamanaji leo Jumanne asubuhi.

“Mashambulizi haya hayakubaliki,” alisema katika chapisho kwenye X (zamani Twitter), akiongeza kwamba waandamanaji “walisababisha moto ambao sasa umedhibitiwa”.

Moshi mwingi ulionekana ukifuka kutoka kwa ubalozi wa Ufaransa, baada ya sehemu yake kuchomwa moto.

“Kila kitu kinafanywa ili kuhakikisha usalama wa mawakala wetu na raia,” Barrot aliongeza.

Waandamanaji pia walilenga balozi za Rwanda, Uganda, Ubelgiji, Uholanzi na Marekani.

Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa,UN unasema hospitali zimezidiwa na mamia ya majeruhi kufuatia vita vya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wanaodaiwa kuuteka mji huo kutoka kwa jeshi la Congo.

Kuna ongezeko la miito kwa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzisha tena mazungumzo ya amani.

Waasi wa M23 wanasema kuwa sasa wameuteka uwanja wa ndege wa Goma. Wamekuwa wakikabiliwa na upinzani lakini wanaonekana kukaribia kuudhibiti mji wote.

UN inasema kuna miili ya watu waliokufa mitaani na kuna ripoti za ubakaji uliofanywa na wapiganaji.

Zaidi ya kilomita elfu mbili kutoka mji mkuu wa Congo, Kinshasa, watu wamekasirishwa na shambulio hilo la waasi.

Majirani wa nchi hiyo Uganda na Rwanda wana historia ndefu ya kuunga mkono makundi ya waasi mashariki.

Balozi zao ni miongoni mwa zile ambazo zilishambuliwa na kuporwa. Kuna hatari ya kutokea mzozo wa kikanda, marais wa Congo na Rwanda wametakiwa kujaribu mazungumzo ya amani.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *