Wakuu wa jeshi la Ethiopia na wale wa eneo lililojitenga la Somaliland, wamekuwa wakijadiliana kuhusu ushirikiano wa kijeshi huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu makubaliano ambayo yanaweza kuipa Ethiopia kambi ya jeshi la wanamaji kwenye Ghuba ya Aden.
Pande hizo mbili zilitia saini mkataba Januari mosi, ili kuipa Ethiopia fursa ya kibiashara na kijeshi baharini.
Somalia ilikiita kitendo hicho kuwa cha uchokozi. Inachukulia Somaliland kama sehemu ya eneo lake na imeapa kutetea uhuru wake.
Somaliland iliyokuwa chini ya ulinzi wa Uingereza, ilijitenga kutoka Somalia mwaka 1991 lakini haitambuliwi kimataifa kama taifa huru.
Mkuu wa jeshi la Ethiopia Birhanu Jula alizungumza na Meja Jenerali wa Somaliland Nuh Ismael Tani kuhusu “njia zinazowezekana za kufanya kazi pamoja” katika mkutano wa Jumatatu Jijini Addis Ababa, jeshi la Ethiopia lilisema katika taarifa.
Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.