Wakulima wa majani chai katika kaunti ya Kakamega, wamehimizwa kuongeza uzalishaji majani chai kutoka kilo milioni tatu kwa sasa, hadi kilo milioni tano kwa mwaka.
Mkurugenzi wa shirika la ustawi wa majani chai humu nchini (KTDA) Alung’ana Khasiani aliyewakilisha eneo la 12, alisema kampuni hiyo itashirikiana na serikali ya kaunti ya Kakamega kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji tayari kwa kiwanda cha majanichai ambacho kimetarajiwa kwa muda mrefu.
Haya yanajiri huku mtandao wa utafiti na utawala (NRG) ambalo ni shirika la kijamii (CSO) katika kaunti hiyo, likielekeza kidole cha lawama kwa kaunti hiyo kwa utepetevu katika shughuli ya ujenzi wa kiwanda cha majanichai licha ya mgao wa ujenzi kila mwaka.
Ujenzi wa kiwanda hicho ulizinduliwa na aliyekuwa gavana Wycliffe Oparanya wakati wa kipindi chake cha uongozi baada ya ahadi yake kwa wakazi kupitia manifesto yake.
Mkurugenzi wa NRG Paul Odongo alisema shirika lake linasukuma serikali ya kaunti, likitaka kujua ni kwa nini imechukua muda mrefu kujengwa kwa kiwanda hicho huku serikali hiyo ikitenga fedha za ujenzi wa mradi huo kila mwaka wa kifedha.
Wakulima sasa wanadai mradi huo umegeuzwa na wanasiasa wengi kuwa mbinu ya kufanyia kampeni, akimtaka gavana aliye uongozini Fernandes Barasa kuhakikisha mradi huo umekamilika.