Wakulima wagawiwa mbegu Nyandarua

Martin Mwanje
1 Min Read

Mvua kubwa inayonyesha katika maeneo mbalimbali nchini imemfanya Gavana wa kaunti ya Nyandarua Kiarie Badilisha kuanzisha kampeni ya kuwawezesha wakulima kupitia ugavi wa mbegu za mahindi na maharagwe za muda mfupi zitakazopandwa wakati wa kindi hiki cha mvua. 

Badilisha amesema maeneo mengi katika kaunti hiyo hasa katika kaunti ndogo ya Ndaragwa yameshuhudia kushindwa kukua kwa mimea kutokana na ukosefu wa mvua na kuna haja ya kutumia mvua ya sasa kupanda mbegu zinazozalisha mazao kwa muda mfupi.

Gavana huyo aidha aliwataka wakazi kupanda mimea mbalimbali badala ya kutegemea kilimo cha viazi pekee kwani mimea mingine kama vile pareto pia inaweza kuwa na manufaa ya kiuchumi.

Aliyasema hayo katika kijiji cha Muthiga katika wadi ya Leshau Pondo alikowahakikishia wakazi juu ya kujitolea kwake kutimiza ahadi alizotoa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita kuhusiana na masuala ya afya, elimu, kilimo na utawala.

Share This Article