Wakfu wa M-pesa kulipa KRA shilingi milioni 6.5

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakfu wa M-pesa kulipa KRA shilingi milioni 6.5.

Wakfu wa M-Pesa utailipa halmashauri ya kukusanya ushuru nchini KRA, malimbikizi ya ushuru ambayo ni jumla ya shilingi milioni 6.5.

Hii inafuatia uamuzi uliotolewa na jopo, lililotupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na wakfu huo kupinga malimbikizi hayo ya ushuru.

Kulingana na halmashauri ya KRA, wakfu wa M-Pesa, uliingia katika makubaliano na kampuni ya Safaricom, ambapo Safaricom iliwahamisha wafanyakazi wake kwa wakfu huo na kuitoza ada iliyotokana na mchakato huo.

Mpangilio huo ulichukuliwa kuwa uhusiano wa anayetoa huduma na anayepokea huduma, huku huduma zilizotolewa zikiorodheshwa kuwa za usimamizi na kitaalam, kulingana na KRA.

Huku likikubaliana na halmashauri ya KRA, jopo hilo lilidokeza kuwa kuliwa na mkataba kati ya M-pesa na Safaricom kwa utoahi wa huduma za wafanyakazi.

Jopo hilo lilisema malipo kutoka kwa M-pesa hadi kwa Safaricom, yalijumuisha mapato ya Safaricom.

Kwa mujibu wa sheria, mtu anapolipia huduma za mkataba, anapaswa kuondoa asilimia 5 na kulipa halmashauri ya KRA.

Share This Article