Ramaphosa amjibu Trump kuhusu hatua ya kukata ufadhili kwa nchi yake

BBC
By
BBC
2 Min Read
Cyril Ramaphosa - Rais wa Afrika Kusini / Picha kwa hisani ya Reuters

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini ni demokrasia ya kikatiba ambayo imekita mizizi katika utawala wa sheria, haki na usawa. Amesema serikali ya Afrika Kusini haijanyakua ardhi yoyote.

Ramaphosa alikua akijibu matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alisema atakata ufadhili wa nchi yake kwa Afrika Kusini.

Rais huyo wa Marekani alisema jana Jumapili, bila kutaja ushahidi, kwamba “tabaka fulani za watu” nchini Afrika Kusini wamekuwa wakitendewa “vibaya sana” na kwamba atakata ufadhili kwa nchi hiyo hadi suala hilo litakapochunguzwa.

“Afrika Kusini inanyakua ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani vibaya sana,” Trump alisema kwenye chapisho la mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

“Marekani haitanyamaza kwa hilo, tutachukua hatua. Pia, nitakata ufadhili wote ujao kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii utakapokamilika!”, alisema Trump.

Akijibu hayo kupitia ujumbe wake kupitia mtandao wa X, Ramaphosa amesema sheria ya unyakuzi iliyopitishwa hivi majuzi si chombo cha kutaifisha, bali ni mchakato wa kisheria ulioidhinishwa kikatiba ambao unahakikisha upatikanaji wa ardhi kwa umma kwa njia ya usawa na haki kama inavyoelekezwa na katiba.

“Afrika Kusini, kama Marekani na nchi nyinginezo, daima imekuwa na sheria za unyakuzi ambazo zinasawazisha hitaji la matumizi ya ardhi ya umma na ulinzi wa haki za wamiliki wa mali,” alisema Ramaphosa.

“Tunatazamia kushirikiana na utawala wa Trump kuhusu sera yetu ya mageuzi ya ardhi na masuala yenye maslahi baina ya nchi mbili. Tuna hakika kwamba kati ya shughuli hizo, tutashiriki uelewa bora na wa pamoja juu ya mambo haya.”

Licha ya misaada ya PEPFAR, ambayo inajumuisha 17% ya programu ya UKIMWI ya Afrika Kusini, hakuna ufadhili mwingine unaopokelewa Afrika Kusini kutoka Marekani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *