Wanariadha watatu wa Kenya wameteuliwa kuwania tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka katika mbio za barabarani katika tuzo za Shirikisho la riadha zitakazoandaliwa Disemba mwaka huu.
Walioteuliwa ni Ruth Chepngetich, Agnes Jebet Ng’etich na Benson Kipruto .
Chepng’eticha amteuliwa baada ya kushinda makala ya mwaka huu ya mbio za Chicago Marathon akiweka rekodi mpya ya Dunia ya saa 2 dakika 9 na sekunde 56.
Agnes Ng’etich amejumuishwa katika orodha ya wanariadha watano wa mwisho baada ya kuweka rekodi mpya za Dunia katika mbio za kilomita 5 na 10, na pia kuweka muda wa kasi katika mbio za nusu marathon.
Wakenya hao wanawania tuzo hiyo pamoja na Sutume Asefa Kebede wa Ethiopia, aliyeshinda Tokyo Marathon mwaka huu, Sifan Hassan wa Uholanzi aliyeshinda dhahabu ya marathon ya Olimpiki na Tigist Ketema aliyeshinda mbio za Berlin Marathon.
Benson Kipruto anawania tuzo ya wanaume baada ya kutwaa ubingwa wa Tokyo marathon na kunyakua nishani ya shaba ya Olimpiki katika marathon.
Kipruto anashindania tuzo hiyo pamoja na Yomif Kejelcha,wa Ethiopia aliyeweka rekodi mpya ya Dunia ya nusu marathon,Jacob Kiplimo,wa Uganda aliyenyakua dhahabu ya Dunia ya mbio za nyika na kushinda Valancia 10km, Brian Daniel Pintado,wa Ecuador aliyeshinda dhahabu ya Olimpiki katika kilomita 20 matembezi na Tamirat Tola,wa Ethiopia aliyetwaa ubingwa wa Olimpiki katika marathon.
Upigaji kura utafungwa Novemba 3 kupitia kwa mitandao ya kijamii ya Shirikisho la Riadha Duniani.