Kuna haja kwa Wakenya kushikana mikono ili kupambana na jinamizi la pombe haramu na dawa za kulevya humu nchini.
Hayo yamesemwa na mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi wakati akizungumza katika kaunti ya Meru.
Amepongeza jitihada za Rais, Naibu Rais, wabunge na wawakilishi wadi kufuatia juhudi zao za kutokomeza jinamizi hilo.
“Rais, Naibu Rais, wabunge na wawakilishi wadi wanafanya kazi ngumu na kushinikiza kutekelezwa kwa sheria za kupunguza vifo vilivyokithiri vya watoto wavulana. Pombe na dawa za kulevya zimesababisha vifo vingi. Lazima tuungane kama wanawake na wazazi ili kuwaokoa watoto wetu na kuondoa dawa kwenye miili yao, kuwapenda ili warejee nyumbani na wawe sehemu ya raia wanaojenga taifa,” alisema Dorcas.
Aliwapongeza watumishi wa Mungu kutoka dini zote za Kikrito, Kiislamu na Kihindu kwa kufungua vituo vya kurekebisha tabia watoto wavulana na wanaume waliopotelea mitaani kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.
Serikali imeapa kukabiliana vilivyo na matumizi ya pombe haramu na mihadarati nchini ambayo yamesababisha kuyumba kwa maisha ya vijana wengi nchini huku Mlima Kenya na maeneo mengi ya Pwani yakiathiriwa.
Mkewe Naibu Rais anaongoza juhudi za kuhakikisha matumizi ya bidhaa hizo yanakomeshwa.