Wizara ya Afya imewataka Wakenya kuchukua tahadhari kutokana na ongezeko la visa vya mafua katika maeneo kadhaa nchini.
Kwenye taarifa, wizara inasema ongezeko hilo linawiana na mienendo inayofahamika ya mafua ya msimu inayotokea kati ya mwezi Februari na Mei na Julai na Oktoba kila mwaka.
“Wizara inaendelea kufuatilia hali kwa karibu kupitia uangalizi ulioimarishwa na mwitikio kwa mabadiliko yoyote katika mienendo ya ugonjwa huo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth kwenye taarifa.
“Watu wengine walioambukizwa wanakumbwa na ugonjwa usiokuwa mkali hadi wa kati na wanapona vizuri kutokana na huduma za matibabu wanazopewa.”
Data za uchunguzi kutoka kwa Mfumo wa Taifa wa Uchunguzi wa Mafua kwa sasa zinaonyesha maambukizi ya kiwango cha juu kuliko wastani yanayoendana na mienendo ya msimu.
Mafua almaarufu Influenza ni maambukizi ya virusi ya mfumo wa upumuaji yanayoenea haraka kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia vitone vinavyotolewa mtu aliyeambukizwa anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza.
Mtu anaweza pia akaambukizwa akikaribiana na mtu aliyeambukizwa na kugusa vitu vilivyo na virusi vya ugonjwa huo na kisha kugusa mdomo, pua au macho.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kushikwa na homa ghafla, kikohozi kikavu, koo linalowasha, kutiririkwa na makamasi au pua kuziba, kichwa kuuma, maumivu ya misuli na viungo na mwili mzima kuwa dhaifu kwa ujumla.
Watu walio katika hatari ya kuambukiziwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wazee, wajawazito na watu walio na matatizo ya kiafya kama vile ugonjwa wa kisukari, saratani na kingamwili dhaifu.
Hatua za kijikinga zinajumuisha kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara, kufunika mdomo na pua unapokohoa au kupiga chafya, kuepuka kutangamana na watu wenye dalili kama za mafua na kuvaa barakoa ikiwa una dalili hizo.