Wakenya wapinga kuongezwa kwa mshahara wa wabunge

Martin Mwanje
2 Min Read

Taarifa kuwa maafisa wakuu wa serikali wakiwemo Maspika wa Bunge la Taifa na Seneti, Wabunge, Maseneta, Mawaziri na Makatibu wao wataongezwa mshahara kuanzia mwezi huu zimekumbana na wimbi la pingamizi kali kutoka kwa Wakenya. 

Katika mitandao ya kijamii, pingamizi zimezagaa huku Wakenya wakilaani hatua hiyo ambayo wameitaja kuwa ya kibinafsi hasa wakati huu ambapo uchumi wa taifa unachechemea.

Wala si Wakenya tu wanaopinga pendekezo la Tume ya Mishahara na Marupurupu kuwaongezea wabunge na maafisa wengine wakuu serikalini mshahara.

Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo amekashifu hatua hiyo akiitaja kuwa isiyostahili.

“Kuongezwa kwa mishahara ya maafisa wa serikali wakiwemo Magavana halistahili kabisa kwa wakati huu,” amesema Orengo ambaye wakati mmoja alihudumu kama Seneta wa kaunti ya Siaya.

Aliyekuwa Seneta mteule Millicent Omanga pia amepinga vikali pendekezo la kuwaongezea wabunge na maafisa wengine serikalini mshahara akisema isitoshe mishahara yao inapaswa kupunguzwa.

“Ni usaliti kwa Wakenya kwa mishahara na mafao mengine ya maafisa wa serikali kuongezwa kwa wakati huu ambapo kuna shinikizo la mishahara hiyo kupunguzwa,” alisema Omanga ambaye aligombea wadhifa wa Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Nairobi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ingawa hakufanikiwa.

“Hatuwezi daima kuwachukulia Wakenya kuwa wajinga. Punguza, wala usiongeze. Hicho ndicho wanachokitaka Wakenya!!!.”

Ikiwa pendekezo la SRC la litatekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 ulioanza Julai Mosi mwaka huu, basi mshahara wa Maspika wa bunge la Taifa na Seneti utaongezwa hadi shilingi 1,208,362 kutoka shilingi 1,185,327, ya Mawaziri na Magavana itaongezwa hadi shilingi 990,000 kutoka shilingi 957,000 huku mshahara wa Naibu Spika ukiongezwa hadi shilingi 966,690 kutoka shilingi 948,261.

SRC pia imependekeza kuongezwa kwa mshahara wa Makatibu kutoka shilingi 792,519 hadi 819,844, viongozi wa walio wengi na wachache kutoka shilingi 784,768 hadi 800,019, Wabunge na Maseneta kutoka shilingi 725,502 hadi shilingi 739,600 huku tume hiyo ikipendekeza mshahara wa Wawakilishi Wadi kuongezwa kutoka shilingi 154,481 hadi shilingi 164,588.

Website |  + posts
Share This Article