Kamishna wa Ulinzi wa Data Immaculate Kassait amewaonya Wakenya dhidi ya kushirikishana taarifa za kibinafsi za watu bila idhini ya watu hao.
Katika taarifa, Kassait ametaja hatua hiyo kuwa kinyume cha Kifungu Nambari 31 cha Katiba, Sheria ya Ulinzi wa Data ya mwaka 2019 na sheria zingine husika.
“Ofisi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data (ODPC) imebaini kuwa kumekuwa na mwenendo wa kukusanya na kushirikishana taarifa za kibinafsi (majina, nambari za rununu, maeneo na maelezo ya kina ya jamaa) wa kundi fulani la raia kupitia mitandao ya kijamii,” alisema Kassait katika taarifa leo Jumatano ambayo haikuwataja wabunge moja kwa moja.
“Kutokana na hilo, Ofisi hii ingependa kuushauri umma kuepukana na kushirikishana zaidi taarifa za kibinafsi kunakoingilia haki za faragha za watu ambao taarifa zao zimeshirikishwa.”
Aidha, amewataka watu ambao taarifa zao zilishirikishwa kuwasilisha malalamishi yao kwa ofisi yake.
Taarifa hiyo inakuja bada ya Wakenya kushirikishana nambari za simu za mkononi za wabunge na kisha kuwatumia jumbe za kuwataka kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la taifa Kuria Kimani na kiranja wa wengi Silvanus Osoro ni miongoni mwa wabunge waliokiri kutumiwa jumbe lukuki za kuwataka kupinga mswada huo.
Hata hivyo, wawili hao ni miongoni mwa wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wanaounga mkono Mswada wa Fedha 2024.