Wakenya zaidi ya milioni 26 wamejisajili SHA, asema Waziri Duale

Duale pia amesema jumla ya shilingi bilioni 70 zimekusanywa kupitia mpango huo, fedha ambazo zimechangwa na watu milioni 4.4.

Dismas Otuke
1 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya

Jumla ya Wakenya milioni 26.5 wamejisajili kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kufikia sasa. 

Waziri wa Afya Aden Duale pia amesema jumla ya shilingi bilioni 70 zimekusanywa kupitia mpango huo, fedha ambazo zimechangwa na watu milioni 4.4.

Duale anasema huduma zinazotolewa chini ya SHA sasa zinapatikana katika vituo vya afya zaidi ya 10,000 huku Wakenya zaidi ya milioni 17 wakivitembelea vituo hivyo kutafuta huduma za matibabu.

“Hadi kufikia sasa, shilingi bilioni 59.3 zimesambazwa kupitia Bima ya Afya ya Jamii (SHIF),” alisema Duale alipohudhuria Kikao cha Kawaida cha 28 cha Baraza la Bajeti na Kiuchumi baina ya Serikali (IBEC) katika makazi rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, Nairobi leo Jumatatu.

Aidha, Wizara ya Afya inasema imewasajili wahudumu wa afya ya jamii 100,193 katika hatua inayolenga kuleta uwazi katika malipo na ujumuishaji wa wahudumu hao kwenye mitambo ya kidijitali.

Wizara hiyo inasema hatua hiyo imepiga jeki afya ya msingi kwa jamii.

 

Website |  + posts
Share This Article