Rais Ruto: Kenya itashinikiza mabadiliko katika sekta ya fedha ya kimataifa

Tom Mathinji
2 Min Read

Kenya itaendelea kutetea mabadiliko katika sekta ya kifedha ya kimataifa, ili iwezwe kuzingatia ipasavyo mahitaji ya mataifa yanayostawi.

Rais  William Ruto alisema itakuwa muhimu kuangazia deni kubwa linalodaiwa mataifa hayo na jinsi litakavyolipwa ili kuhakikisha kwamba mataifa hayo hayashindwi kuilipa madeni yake, hasa wakati yanapokumbwa na mikasa na majanga ya magonjwa.

Kiongozi wa taifa alisema hayo wakati alipohutubia kupitia mtandao, mkutano wa vugu vugu la viongozi wa serikali kuhusu maendeleo, ulioandaliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa  Antonio Guterres.

Mkutano huo wa ngazi za juu utafuatiwa na kongamano la nne la kimataifa kuhusu ufadhili wa kimaendeleo huko Seville nchini Uhispania baadaye mwezi huu.

Awali Rais Ruto alikutana na balozi wa Uingereza humu nchini Neil Wigan,katika ikulu ya Nairobi, ambapo alisema Kenya inachunguza upya mikakati ya ushirikiano baina yake na Uingereza  kuambatana na ajenda za serikali za mataifa hayo mawili.

Kenya na Uingereza zitaimarisha ushirikiano wao katika maswala ya mabadiliko ya hali ya anga,uhifadhi wa mazingira, sayansi na teknolojia,amani na usalama pamoja na biashara na uwekezaji.

Kiongozi wa taifa alisema ushirikiano huo pia utajumuisha utekelezaji wa mradi wa huduma za reli hapa Nairobi,upanuzi wa mradi wa uzalishaji umeme kupitia miyale ya jua huko Malindi pamoja na ushirikiano katika sekta ya usalama wa mitandao na juhudi za kukabiliana na ugaidi miongoni mwa maswala mengine.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article