Usafiri kwenye barabara ya Ruiri–Isiolo, iliyo kwenye mpaka wa kaunti za Meru na Isiolo, ulisimama kwa muda baada ya wakazi kuandamana wakilalamikia kuongezeka kwa visa vya ukosefu wa usalama na wizi wa mifugo.
Waandamanaji hao waliziba barabara kwa mawe na miti ya miiba, wakitaka serikali ichukue hatua dhidi ya wavamizi wa mifugo waliotekeleza uvamizi wiki mbili zilizopita. Wakazi wanadai kuwa mifugo hao zaidi ya ng’ombe na mbuzi 125 walipelekwa hadi kaunti ya Samburu.
Waandamanaji walikabiliana kwa muda na polisi waliokuwa wakijaribu kuwatawanya.
Mwanaharakati wa kisiasa kutoka Meru, Mike Makarina, alijiunga na waandamanaji hao na kuwalaumu maafisa wa serikali kwa kuwavunja moyo wananchi waliokuwa wakijaribu kurejesha mifugo wao, licha ya kuwa walifuata nyayo za mifugo hadi Samburu ambako wanadaiwa kufichwa.
Makarina alijitokeza kumuunga mkono mmoja wa waathiriwa wa wizi huo, Junice Kaulu, mwanamke mlemavu mwenye umri wa miaka 40, ambaye alipoteza zaidi ya ng’ombe na mbuzi hamsini.
“Serikali isiketi tu ikiwa kimya. Tunajua wizi huu umetendwa na watu maalum, na mifugo hiyo imeshafuatwa hadi ilipo. Tunahitaji hatua, si maneno,” alisema Makarina.
Alimtaka Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen kuachilia rasilimali za kutosha ili kusaidia katika msako wa wahalifu hao.
Waandamanaji pia waliishutumu serikali kwa kusita kuchukua hatua licha ya ushahidi uliopatikana katika tukio hilo simu ya mkononi na kitambulisho vilivyoachwa na wavamizi hao wakati wa msako uliofanywa na wananchi kwa kushirikiana na Polisi wa Akiba (KPR).
Peter Kailemia, mkazi mwingine aliyeathirika, alisema familia tatu zilipoteza mifugo kwenye uvamizi huo. Alilalamikia hatua ya maafisa wa usalama waliokuwa ndani ya gari la kivita kukataa kukabiliana na wavamizi waliokuwa na mifugo hiyo.
“Maafisa walikataa kutoka kwenye gari lao hata tulipowaomba msaada. Mifugo yetu ilienda tu mbele ya macho yao,” alisema Kailemia.
“Tunaomba serikali ichukue hatua madhubuti.”
Kaulu alisema huu ulikuwa ni uvamizi wa tatu kumkumba, lakini katika visa vya awali, serikali iliweza kusaidia kurejesha mifugo. Safari hii, anahofia mambo ni tofauti.
Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai kutoka Buuri Mashariki waliwataka wakazi kuwa na subira huku wakisema uchunguzi wa kijasusi umeanza. Walisema ushahidi uliopatikana, ikiwemo kitambulisho na simu ya mkononi, utasaidia kuwafichua waliopanga na kutekeleza wizi huo.