Wakazi wa Nyandarua wahimizwa kukumbatia kilimo cha Tufaha

Tom Mathinji and Lydia Mwangi
2 Min Read
Tunda la Tufaha (Apple).

Kilimo cha tufaha kinazidi kupata umaarufu hapa nchini, kutokana na ongezeko la hitaji lake katika soko la hapa nchini.

Ongezeko la hitaji la tunda hilo, limesababishwa na manufaa yake ya kiafya na faida zake za kifedha.

Matunda mengi ya Tufaha yanayopatikana hapa nchini, yameagizwa kutoka Afrika Kusini, huku kilimo chake hapa nchini kikianza kushika kasi.

Hali nzuri ya hewa katika kaunti ya Nyandarua, inatoa mazingira mwafaka ya ukuzaji wa tunda hilo ambalo humezewa mate na wengi.

Ni kwa misingi hii ndiposa Gavana wa kaunti ya Nyandarua Dkt. Kiarie Badilisha anapigia debe ukulima wa zao hilo, akisema serikali yake itatumia kitita cha shilingi milioni 26 kwa ukulima wa tunda hilo.

Gavana Badilisha azuru shamba la Tufaha kaunti ya Nyandarua.

Akizungumza alipozuru shamba la tufaha katika kijiji cha Ngorika, eneo la Olkalou, Gavana Badilisha alisema zao hilo halitapanua tu shughuli za kilimo, lakini pia litasababisha wakulima wa eneo hilo kuongeza mapato yao.

Aliwahimiza wakulima zaidi kukumbatia kilimo cha tufaha, hususan baada ya serikali yake kuahidi kuwasaidia wakulima, ili kuwawezesha kuongeza mapato yao na hivyo kuinua sekta ya kilimo katika kaunti hiyo.

Kwa upande wake, mkulima wa tufaha katika eneo hilo John Ndegwa, alisema mkulima anaweza pata faida ya hadi shilingi 200,000 iwapo masharti ya upanzi wa tunda hilo utazingatiwa kikamilifu.

Kulingana na mkulima huyo, mti wa tufaha huhitaji kunyunyiziwa maji mara kwa mara, hasaa katika miaka ya kwanza ya upanzi na nyakazti za joto na anga kavu.

Mti wa tufaha huchukua muda wa miezi 11 kuanza kuzaa matunda, iwapo masharti ya upanzi yatazingatiwa.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article