Wakazi wa eneo bunge la Mwea katika kaunti ya Kirinyaga, watanufaika na ujenzi wa vituo vya Huduma Centre na kitovu digitali (jitume digital Hub) ambavyo ujenzi wake umeanza leo Ijumaa.
Mradi huo ambao utagharimu shilingi milioni 24, unatarajiwa kukamilika mwezi wa pili mwaka kesho na kuleta huduma ya serikali karibu na wananchi huku ukiinua matumizi ya digitali katika eneo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, mjumbe wa mwea – Mary Maingi, alisema kuwa, “Wakaazi wa Mwea hawatasafiri mbali kupata huduma ya serikali. Kituo hiki kitapunguza usafiri wa mara kwa mara na kuboresha huduma”. Alisema Maingi.
Aliongeza kuwa afisi yake ya hela za NG-CDF itasaidia mradi huo – Jitume Hub kwa kununua tarakilishi kwa kuwa serikali ya Kenya kwanza imejisatiti kusaidia vijana kujitegemea kupitia digitali.
Kauli hiyo iliungwa mkono na naibu kamishina wa kaunti hiyo – Purity Mengich aliyesisitiza kuwa mpango huo ni ishara ya bidii ya serikali ya kutoa huduma kwa wananchi haswa walio mashinani, hivyo akawataka vijana kutumia fursa hiyo kujinufaisha.
Naye mkaazi wa eneo hilo – Titus Karanja hakuficha furaha yake kwa maneno kuwa, “ Tumekuwa tukienda mjini Kerugoya na katika kaunti ya Embu kupata huduma ya serikali unapohitaji na imekuwa vigumu na ghali kwetu na yenye kutumia muda mrefu kwa sababu tunatumia siku nzima”. Alinena Karanja.
Fauka ya hayo, Maingi aliwatakia heri njema watahiniwa wote wa Mwea na taifa nzima.